Viongozi wanawake watakiwa kubadilisha taasisi, kupanua upatikanaji wa haki

Msajili mkuu wa idara ya mahakama Winfridah Mokaya alisema wanawake katika Mahakama wanaongoza mageuzi ya kitaasisi, mabadiliko ya kidijitali na ubunifu.

Marion Bosire
1 Min Read

Msajili mkuu wa idara ya mahakama Winfridah Mokaya amewataka viongozi wanawake kutumia nyadhifa zao kubadilisha taasisi, kuimarisha haki za kijinsia na kupanua upatikanaji wa haki.

Akizungumza katika kongamano la shirika la mawakili wanawake FIDA Kenya uliokuwa na kaulimbiu “Wanawake Waongoza Kupitia Mabadiliko: Haki za Kijinsia, Ubunifu wa Kidijitali na Ushiriki wa Kidemokrasia,” Mokaya alisema maendeleo ya wanawake yamejengwa juu ya ustahimilivu na kujitolea kwa vizazi vilivyotangulia.

Alisema wanawake katika Mahakama wanaongoza mageuzi ya kitaasisi, mabadiliko ya kidijitali na ubunifu.

Alisisitiza kuwa teknolojia inapaswa kuboresha ufanisi na upatikanaji wa haki bila kuunda vikwazo vipya kwa wanawake wasio na simu za kisasa, intaneti ya kuaminika au ujuzi wa kidijitali.

Mokaya pia alieleza mageuzi yanayotokana na matumizi ya data, yakiwemo kuweka kidijitali Sajili ya Wahalifu Waliopatikana na Hatia za Makosa ya Kijinsia, ambayo imerekodi hukumu 10,894.

Aidha, alitaja mageuzi katika masuala ya mirathi, ambapo Barua za Usimamizi wa Mirathi sasa zinalengwa kushughulikiwa ndani ya siku 60.

Mokaya alitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya FIDA Kenya na Mahakama katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia na kukuza haki za kidijitali zinazowafikia wote.

Share This Article