Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kambe Ribe, kaunti ya Kilifi wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na wizi wa pikipiki mbili ambazo zimepatikana.
Wakati wakishika doria kwenye barabara ya Kipara Mwakirunge huko Kaloleni, maafisa hao waliarifiwa na mkazi mmoja kwamba ameibiwa pikipiki nyumbani kwake.
Ni taarifa iliyowachochea maafisa hao kuanzisha operesheni haraka ya kuitafuta pikipiki hiyo.
Operesheni hiyo ilifanikisha kupatikana kwa pikipiki hiyo pamoja na nyingine ambayo pia inaaminika kuibiwa.
Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS inasema washukiwa hao watatu kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kambe Ribe wakisubiri kufikishwa mahakamani.