Mahakama moja mjini Mombasa imewahukumu wanaume wawili kifungo cha miaka saba gerezani kila mmoja, kwa kuhusika katika wizi wa bunduki aina ya AK-47 ya afisa wa polisi na risasi 30 wakati wa shambulizi la usiku katika eneo la viwandani la Bonje huko Jomvu, kaunti ya Mombasa.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya upande wa mashitaka ukiongozwa na Godfrey Ngigi, kuwasilisha ushahidi wa kutosha unaowahusisha Pius Oketch na Kellas Wanyonyi na wizi huo.
Mahakama ilifahamishwa kuwa, genge moja lilimshambulia konstebo wa polisi James Kobia, aliyekuwa akilinda kiwanda cha industrial park akiwa pamoja na walinzi wa kibinafsi. Afisa huyo alizidiwa nguvu na kuibiwa bunduki aina ya AK 47 ikiwa na risasi 30. Mmoja wa walinzi wa kibinafsi pia aliibiwa simu ya mkononi.
Siku tatu baada ya wizi huo, maafisa wa polisi walimkamata Wanyonyi, ambaye baadaye aliwapeleka maafisa hao hadi nyumbani kwa Oketch katika mtaa wa Narcol. Polis walimpata Oketch akiwa amejificha kwenye paa la nyumba, na baada ya upekuzi walipata bunduki hiyo na risasi 30 zikiwe ndani ya gunia.
Hakimu Mkuu Hamlick Muriithi Mwenda aligundua kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha kesi yake bila shaka yoyote. Mahakama ilitaarifiwa kwamba genge hilo lilimshambulia konstebo James Kobia, ambaye alikuwa akilinda eneo hilo pamoja na walinzi wa kibinafsi.
Hakimu huyo alitupilia mbali ya washtakiwa hao kwamba walisngiziwa na maafisa wa polisi.
Washtakiwa wote wawili walishauriwa kuhusu haki yao ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo katika muda wa siku 14.