Familia yalilia haki kufuatia kifo cha kijana wao Murang’a

KBC Digital News
3 Min Read

Familia ya kijana mwenye umri wa miaka 23 aliyedaiwa kuuawa na maafisa wa polisi karibu na ua wa shamba la Del Monte, huko Del View, kaunti ya Murang’a sasa inataka kufanywa kwa uchunguzi huru kubaini hali aliyokumbana na mauti.

Aidha, inataka afisa aliyefyatua risasi na kumuua kijana huyo kutambuliwa na kuwajibishwa.

Peter Kimani Gitau alipigiwa risasi majira ya saa tisa usiku Jumamosi iliyopita wakati akiwa ameandamana na vijana wengine waliojaribu kuingia kwenye shamba la Del Monte ili kuiba mananasi.

Kifo chake kilisababisha kuchacha kwa maandamano kwenye barabara kuu ya Thika-Kenol Jumamosi asubuhi.

Baadhi ya waandamanaji waliripotiwa kuwaibia wasafiri na kutatiza usafiri kabla ya polisi kuingilia kati.

Binamu ya Kimani, Esther Njeri, amesema familia ilipigiwa simu majira ya saa tisa usiku ikiarifiwa kwamba jamao wao amepigwa risasi. Ni simu iliyowafanya kukimbia hadi hospitali binafsi huko Kenol ambako kijana huyo alikimbizwa ili kutibiwa ila akafariki.

Njeri anasema awali familia haikuweza kubaini ni nini hasa kilichosababisha kifo chake, lakini ilitambua kile kilichoonekana kuwa jeraha kubwa kifuani.

Kulingana naye, familia hiyo ilikumbana na wakati mgumu kupata namba ya OB inayohitajika ili kusafirisha mwili wa Kimani hadi ufuo wa General Kago mjini Thika. Hata hivyo, walifanikiwa baada ya kupokea nyaraka zinazohitajika katika kituo cha polisi cha Kenol ila baada ya usumbufu si haba.

Kiongozi wa jamii Gichango Njuki, aliyejiunga na familia kutoa wito wa kufanywa kwa uchunguzi, alielezea wasiwasi juu ya kufikiwa kwa makubaliano kati ya baadhi ya walinzi wa shamba la Del Monte na vijana wanaojihusisha na wizi wa mananasi.

Njuki alidai baadhi ya vijana wasiokuwa na ajira kutoka maeneo ya Kabati, Makenji na Kenol walifikia makubaliano na walinzi kuingia kwenye mashamba ya mananasi na kuyachukua, na uhusiano kati yao kugeuka kuwa wa kiuhasama punde mizozo ilipoibuka.

Mwanaharakati wa haki za binadamu na Afisa Mkuu Mtendaji wa Vocal Africa, Hussein Khalid pia aliungana na familia hiyo kwenye ufuo wa General Kago katika kutoa wito wa kufanywa kwa uchunguzi kuhusiana na kifo cha Kimani.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa ufuoni hapo ukisubiri kufanyiwa upasuaji wakati familia ikiendelea kudai majibu kuhusiana na kifo hicho.

Taarifa ya KNA

Share This Article