Msimu wa Ligi Kuu Kenya katika mchezo wa soka mwaka 2026/2027 uliokuwa uanze mwishoni mwa juma hili umeahirishwa kufuatia agizo la Mahakama Kuu.
Shirikisho la Soka nchini, FKF lilikuwa limekimbia kortini mapema wiki hii kutaka marufuku hiyo iondolewe ili kupisha kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Jumamosi hii lakini Mahakama ikakataa.
Mzozo huo unafuatia kesi iliyo katika Mahakama Kuu iliyowasilishwa na klabu ya Kariobangi Sharks ya kupinga uamuzi wa jopo la kutatua migogoro michezoni (SDT) wa kuidhinisha mfumo wa kushushwa na kupandisha daraja timu uliopitishwa na FKF.
FKF pia inapinga uhalali wa Mahakama Kuu kusikiza kesi hiyo ikisema kuwa rufaa yoyote dhidi ya uamuzi wa SDT yafaa kuwasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Kutatua Migogoro Michezoni (CAS) nchini Uswizi.
Pande zote zitarejea mahakamani Septemba 21 mwaka huu kwa maelekezo zaidi.
Hatua hii ina maana kuwa msimu wa Ligi ya Kenya huenda uchelewe kuanza kwa zaidi ya mwezi mmoja, hali itakayoathiri kalenda ya msimu humu nchini.
Sharks ilimaliza ya 16 kwenye msimu uliomalizika na hivyo kushushwa ngazi.