Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuhitimisha maonyesho ya kimataifa ya kilimo ya kesho Agosti 8, 2026 katika uwanja wa Dkt John Samuel Malecela Nzuguni Jijini Dodoma.
Maonyesho hayo yalianza Agosti 1 yakihusisha wadau wa sekta za kilimo mifugo na uvuvi.
Kaulimbiu ya maonyesho ya mwaka huu ni ‘Lijue soko ongeza thamani kutekeleza Dira ya 2050’ inayosisitiza umuhimu wa kuelewa masoko kuongeza thamani ya mazao na kutumia teknolojia kukuza sekta ya kilimo.
Washiriki zaidi ya 800 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaowakilisha Nchi 24 wanashiriki maonyesho hayo wakionyesha bidhaa mbali mbali za teknolojia na ubunifu.
Mbegu za mimea inayoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi ndizo zimepatiwa kipaumbele kwenye maonyesho hayo zikifuatiwa na huduma za kidijitali na matumizi ya mitambo ya kisasa.
Maonyesho hayo yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba huku Viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiongoza shughuli za siku maalum za sekta tofauti katika kipindi chote cha maonyesho.
Kilele cha maadhimisho kitafanyika Agosti 8 ambayo ni Siku ya Wakulima ambapo Rais Samia anatarajiwa kutoa hotuba na kusisitiza hatua za Serikali katika kuendeleza kilimo.
Hafla hiyo pia itatoa nafasi kwa Wadau kutathmini mafanikio ya maonesho na kujadili namna ya kuongeza tija na ushindani wa mazao ya Tanzania.