Chama cha Wiper Patriotic Front, kimetangaza mabadiliko katika uongozi wa chama hicho ambapo waziri wa zamani Jamleck Irungu Kamau ameteuliwa kuwa mwenyekiti mpya.
Katika taarifa kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka, alitangaza pia uteuzi wa mbunge wa Nyali Mohamed Ali kuwa Naibu Kiongozi wa Chama mteule na wakili Ndegwa Njiru kuwa msemaji wa kwanza wa chama.
Kalonzo alisema alitekeleza uteuzi huo kutokana na mamlaka aliyopatiwa na wajumbe wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe la chama, ili kupanua na kuhuisha uongozi wa chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Kalonzo alimtaja Kamau kuwa mtaalamu wa kujenga miungano ya kisiasa mwenye uzoefu wa miongo kadhaa, akisema uongozi wake utakiimarisha chama katika juhudi zake za kuunda kile alichokiita “Serikali Mbadala Iliyo Tayari Kuchukua Madaraka.”
Alimpongeza pia Mbunge Mohamed Ali, mwanahabari wa zamani wa uchunguzi, kwa juhudi zake katika kupambana na ufisadi na kuhudumia umma. Alisema analeta uadilifu pamoja na mvuto kwa kizazi cha vijana ndani ya uongozi wa chama.
Wakili Ndegwa Njiru pia aliteuliwa kuwa msemaji wa kwanza wa Wiper Patriotic Front, wadhifa ambao Kalonzo alisema ulibuniwa kwa ajili ya kipindi kipya cha mapambano.
Alimtaja Njiru kuwa mtetezi wa Katiba ambaye amewawakilisha mahakamani wananchi wa kawaida, wabunge na waandamanaji vijana, akiongeza kuwa sasa atakuwa sauti na sura ya chama mbele ya umma.
Kalonzo alisema uteuzi huo umeongozwa na misingi na maadili, si kwa sababu za urahisi wa kisiasa.