Serikali ya Uganda imemtambua kwa njia ya kipekee msanii wa kike wa muziki Sheebah Karungi kutokana na juhudi zake za kutangaza utamaduni wa nchi hiyo.
Karungi alipokezwa tuzo ya Mafanikio ya Watu Mashuhuri kwa Umahiri wa Kipekee katika sanaa na mchango wake mkubwa katika ushawishi wa utamaduni.
Balozi Charles Ssentongo ambaye ni mkurugenzi wa huduma za itikafi katika Wizara ya Mambo ya Nje ndiye alimkabidhi Sheebah tuzo hiyo kwa niaba ya Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje, Harunah Kyeyune Kasolo.
Tuzo hiyo inatambua mchango wa msanii huyo katika kuendeleza na kutangaza utambulisho wa kitamaduni wa Uganda barani Afrika na kwingineko duniani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda ilieleza kuwa utamaduni una nafasi muhimu katika kuimarisha diplomasia, utalii, biashara, uwekezaji na uhusiano imara kati ya nchi za Afrika.
Sheebah Karungi amekuwa akitumia jukwaa lake kuonyesha ubunifu, vipaji na utambulisho wa kitamaduni wa Uganda kwa hadhira iliyo nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Kuanzia maonyesho ya muziki hadi kuiwakilisha Uganda kama sauti ya sanaa yake, Sheebah amejiunga na orodha inayoongezeka ya raia wa Uganda wanaotumia vipaji vyao kuimarisha taswira ya nchi yao katika jukwaa la kimataifa.