Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Uganda Bebe Cool anajiandaa kwa uzinduzi wa albamu yake iitwayo “Break The Chains”.
Akizungumza mubashara kwenye TikTok msanii huyo alifichua kwamba albamu hiyo itazinduliwa rasmi Ijumaa Mei 30, 2025 na kukomesha wasiwasi wa mashabiki zake ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu.
Tayari Bebe Cool amezindua vibao viwili ‘Circumference’ na ‘Motivation’ ambavyo viko kwenye albamu hiyo.
Albamu ya Break The Chains inatarajiwa kuonyesha mchanganyiko wa mtindo asilia wa Bebe Cool na mtindo maarufu wa sikuhizi wa Afrobeats pamoja na simulizi za hadithi.
Cool alisema uamuzi wake wa kuhusisha mtindo wa Afrobeats ulichochewa na mitindo ya sasa ya muziki ulimwenguni ambapo wasanii wengi wanaingilia mtindo wa Afrobeat.
Mashabiki wake hata hivyo walishtuka waliposikia jinsi ameimba wimbo Circumference.
Jina la ‘Break The Chains’ kulingana naye ni la kuashiria jinsi ya kukiuka vikwazo na kujisukuma zaidi na kupita dari ya kioo ambayo kwa miaka mingi imechukuliwa kuwa kikwazo kikuu kwa wasanii wa Uganda kuafikia ulimwengu mzima na kazi zao.
Bebe Cool anaamini kwamba albamu yake mpya itasaidia pakubwa kusukuma muziki wa Uganda hadi katika jukwaa la kimataifa.
Ameshirikisha watayarishaji muziki wapya, wahandisi na wengine katika maandalizi ya albamu hiyo.