Juma Jux asema yuko sawa kukonda

Amesema ameridhika na mwonekano wake wa sasa na hana mpango wa kuongeza uzito.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Juma Jux amesema kwamba yuko sawa na mwili wake mdogo wa sasa baada ya mashabiki kushangazwa na mwonekano wake mpya.

Jux alionekana kwenye harusi ya wanamitandao wa Nigeria Peller na Jarvis akiwa na mke wake ambapo alionekana kama aliyepunguza uzani wa mwili pakubwa kuliko awali.

“Sitaki kuwa mnene, nafurahia kukonda” alisema Jux katika hatua ya kuvunja kimya kuhusu mjadala unaoendelea mitandaoni baada ya mashabiki wengi kuzungumzia kupungua kwake uzito kufuatia picha zake zilizosambaa akiwa kwenye harusi hiyo ya ktamaduni.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Jux amesema ameridhika na mwonekano wake wa sasa na hana mpango wa kuongeza uzito.

“Najipenda hivi nilivyo sasa,sitaki kuwa mnene. Sitaki tumbo langu liwe kubwa. Sitaki kuwa vile” amesema Juma Jux.

Kauli hiyo imezua mijadala mbalimbali mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakimuunga mkono kwa kuamua kuishi maisha yanayompa furaha, na wengine wakieleza walizoea kumuona akiwa na mwili tofauti.

Jux ameoa mwigizaji na mwanamitandao wa Nigeria Priscilla Ojo, ambaye ni binti ya mwigizaji maarufu wa Nigeria Iyabo Ojo, ndiyo sababu yake kualikwa kwa harusi hiyo ya kitamaduni.

Wakati huo huo msanii huyo amehimiza mashabiki zake kuendelea kumpigia kura kwenye tuzo zijazo za AFRIMMA ambapo ameteuliwa kwenye vitengo vitatu ambavyo ni wimbo bora wa mwaka, ushirikiano bora wa mwaka na mwanamuziki bora wa kiume Afrika Mashariki.

Share This Article