Tyrese Gibson awasili Uganda

Anatarajiwa kutumbuiza katika awamu ya pili ya tamasha ya kahawa Oktoba 3, 2026.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki na mwigizaji wa Marekani Tyrese Gibson yuko nchini Uganda ambapo aliwasili leo Jumanne asubuhi akitarajiwa kutumbuiza kama msanii mkuu katika awamu ya pili ya tamasha ya kahawa.

Gibson alitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, ambako alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Talent Africa Group, Aly Allibhai, ambaye kampuni yake inasimamia onyesho hilo.

Nyota huyo wa Hollywood anatarajiwa kutumbuiza katika tamasha ya kahawa, ambayo itafanyika Ntungamo mwezi Oktoba.

Hafla hiyo imeandaliwa na Inspire Coffee Group, iliyoanzishwa na Nelson Tugume na ni sehemu ya juhudi pana za kuitangaza sekta ya kahawa ya Uganda katika jukwaa la kimataifa.

Hii ni mara ya pili kwa Gibson kuzuru Uganda, baada ya kufanya hivyo mwaka 2012, na amefika mapema kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa tamasha hiyo ya Oktoba 3, 2026.

Diamond Platnumz wa Tanzania alikuwa msanii mkuu wa awamu ya kwanza ya tamasha hiyo ya kahawa nchini Uganda ambayo huwa na burudani na mbio za Marathon.

Share This Article