Kesi iliyokuwa ikimkabili mwanamuziki Chris Brown nchini Uingereza imetupiliwa mbali. Hii ni baada ya aliyemshtaki kuamua kuiondoa mahakamani.
Brown alikuwa anakabiliwa na kesi ya kumshambulia mtayarishaji muziki aitwaye Amadou Abe Diaw akitumia chupa ya mvinyo na kumkanyaga katika sehemu moja ya burudani jijini London, Februari mwaka 2023.
Kulingana na Billboard Diaw aliandikia mahakama waraka Ijumaa akiomba kesi dhidi ya Brown itupiliwe mbali bila uwezekano wa kuiwasilisha tena mahakamani.
Haijabainika iwapo wawili hao wameafikiana nje ya mahakama.
Baada ya kushambuliwa na Brown, Diaw alilazwa hospitalini na baadaye akawasilisha kesi mahakamani akidai fidia ya Dola Milioni 16.
Tarehe 15 mwezi Mei mwaka huu wa 2025, Brown alikamatwa kuhusiana na kesi hiyo kutoka hoteli aliyokuwa akilala huko Manchester na kufikishwa katika mahakama ya Southwark Crown jijini London Ijumaa Mei 16, 2025.
Jaji Joanne Hirst alimnyima mwanamuziki huyo dhamana lakini akaridhia ombi hilo baadaye kwa masharti. Aliachiliwa kwa dhamana ya Yuro Milioni 5 ambapo milioni 4 zilistahili kutolewa kabla ya kuachiliwa huku milioni moja ikitolewa katika muda wa siku saba.
Kesi hiyo ilikuwa imehatarisha ziara ya kikazi ya ulimwengu ya Chris Brown iliyopatiwa jina la “Breezy Bowl XX”. Ilianza rasmi Juni 8, huko Amsterdam kabla ya kuelekea maeneo ya Manchester, London, Cardiff, Birmingham na Glasgow mwezi Juni