Zanie Brown adai tasnia ya muziki nchini Uganda inaendeshwa na nguvu za kiroho

Msanii huyo anasema yeye mwenyewe alikumbwa na changamoto ikabidi arejelee Mungu.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Zanie Namugenyi, anayefahamika zaidi kama Zanie Brown, amefunguka kuhusu changamoto za kiroho alizokumbana nazo katika safari yake ya muziki.

Alifichua kuwa wakati wa safari yake alishambuliwa kiroho, jambo lililomsukuma atafute usaidizi wa Mungu. Mwanamuziki huyo alilelewa katika familia ya kikristo na hivyo alimgeukia Mungu kwa ajili ya mwongozo na ulinzi.

Zanie anadai kwamba tasnia ya muziki nchini Uganda inaongozwa na nguvu za giza.

“Hakuna mtu anayepiga muziki bila msaada wa kiroho kutoka kwa Mungu au Shetani. Inakuwa kwamba unaomba au uko kwenye uchawi” alisema mwimbaji huyo.

Alitetea usemi wake akitaja muda aliokaa kwenye tasnia hiyo ambao ni miaka 10 na anafahamu fika kwamba yeyote aliyeno lazima ajitolee kwa upande mmoja.

“Watu wanaoingia kwenye tasnia hii wanapaswa kufahamu jambo hili.” Zania aliendelea kusema akielezea kwamba ingawa baadhi ya wasanii ni wa kiroho sana, huenda wasionyeshe imani yao hadharani.

Zanie anahisi imani yake imeimarika sasa na hana hofu tena kuhusu changamoto alizopitia awali.

Hii sio mara ya kwanza kauli kama hizo zimetolewa na msanii nchini Uganda. Mwanamuziki A Pass aliwahi kusema hataki wasanii wenzake waingie nyumbani kwake kwa kuhofia kuwa wengi wao wanajihusisha na uchawi.

Website |  + posts
Share This Article