Obiri kuwaongoza Wakenya Boston Marathon leo jioni

Mbio hizo zitang'oa nanga mida ya saa kumi leo , na zitakuwa za pili kwenye kalenda ya mbio kuu za Marathon, baada ya Tokyo Marathon.

Dismas Otuke
1 Min Read

Bingwa mara mbili wa Boston Marathon, Hellen Obiri, atalenga kunyakua taji ya tatu leo jioni atakaposhiriki makala ya 129 ya mbio hizo nchini Marekani.

Obiri aliyetwaa ubingwa mwaka 2023 na 2024, atalenga kusawazisha rekodi ya Fatuma Roba wa Ethiopia, aliyeshinda mataji matatu mtawalia miaka 26 iliyopita

Obiri ambaye pia ni mshindi wa nishani ya shaba ya Olimpiki mwaka uliopita atakabiliana na Wakenya wenzake Sharon Lokedi, bingwa mara mbili wa mbio hizo Edna Kiplagat, na Irene Cheptai, miongoni mwa wengine, huku upinzani kwa Wakenya ukitoka kwa bingwa wa dunia Amane Beriso na Yalemzerf Yehualaw, wote kutoka Ethiopia.

Sisay Lemma wa Ethiopia atakuwa akitetea taji ya wanaume akilenga kuwa Mwethiopia wa pili kuhifadhi taji hiyo, ingawa atakuwa na kibarua kigumu kutoka kwa Wakenya John Korir, aliyeshinda Chicago Marathon mwaka jana , bingwa mara mbili wa Boston Marathon Evans Chebet na Daniel Mateiko.

Mbio hizo zitang’oa nanga mida ya saa kumi leo , na zitakuwa za pili kwenye kalenda ya mbio saba kuu  za Marathon, baada ya Tokyo Marathon.

Website |  + posts
Share This Article