Kanye asema yeye na mkewe walishinda tuzo za Grammy

Hii ni baada yao kuangaziwa sana na vyombo vya habari kufuatia mavazi ya Bianca na uvumi kwamba walifukuzwa kutoka kwenye eneo la kutoa tuzo za Grammy.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Kanye West au ukipenda Ye amesema yeye na mke wake Bianca Censori walishinda kwenye hafla ya kutoa tuzo za Grammy.

Ye na Bianca walifika kwenye studio moja huko Los Angeles jana Jumanne Februari 4, 2025 ambapo walikabiliwa na wanahabari.

Kulingana na video inayosambaa mitandaoni, Kanye anasikika akiambia wanahabari hao wamuulize kuhusu jinsi walishinda kwenye tuzo za Grammy.

Mmoja wa wanahabari hao anarudia swali hilo na Kanye anamjibu, “Tulishinda tuzo za Grammy”.

Bianca kwa upande mwingine anaonekana kutojishughulisha na wanahabari hao na anatembea taratibu na kuingia kwenye studio hiyo.

Tofauti na alivyokuwa amevaa kwenye hafla ya tuzo za Grammy, Bianca jana alikuwa amevaa mavazi ya kufunika mwili mzima.

Wakati wa awamu ya 67 ya tuzo za Grammy tarehe 2 mwezi huu wa Februari mwaka 2025 katika ukumbi wa Crypto.com huko Los Angeles, wanandoa hao walizua gumzo.

Hii ni baada yao kufika kwenye ‘Red Carpet’ ambapo walipigwa picha na Bianca akawa amevaa vazi dogo lililoonyesha mwili wake ungedhania yuko uchi.

Baada ya kupigwa picha, wawili hao walikaa muda mfupi na kisha kuondoka hata hawakuingia kwenye ukumbi kwa ajili ya hafla ya tuzo za Grammy.

Baadaye uvumi ulisambaa kwamba walifukuzwa labda kutokana na mavazi ya Bianca lakini baadaye ikabainika kwamba hawakufukuzwa.

Sasa Kanye West anajigamba kwamba walishinda kwa sababu walipata kuangaziwa sana na vyombo vya habari ingawa hakushinda tuzo yoyote ya Grammy siku hiyo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *