Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeshirikiana na Taasisi ya Kuratibu Mtaala nchini (KICD) kujumuisha somo la maadili katika mfumo wa elimu hapa nchini.
Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud amesema hatua hiyo inalenga kuzuia ufisadi na utovu wa maadili kwa kuwalenga vijana wakiwa wangali wachanga, akitambua kuwa mafunzo ya mapema kuhusu maadili husaidia pakubwa katika urekebishaji tabia.
Aliyasema hayo alipomtembelea Mkurugengi ambaye pia ni Afisa Mkuu Mtendaji wa KICD Prof. Charles Ochieng’ Ong’ondo afisini mwake, kuratibu mikakati ya kujumuisha somo la maadili katika mfumo wa elimu.
Viongozi hao wawili walisema kujumuishwa kwa somo la Maadili katika mfumo wa elimu, vijana wa hapa nchini watakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto ibuka na kujiepusha na ufisadi.
Aidha, waliazimia kuimarisha ushirikiano kati ya EACC na KICD kushinikiza mfumo wa elimu unaowapa wanafunzi motisha ya kukumbatia maadili.
Kupitia ukurasa wa X wa EACC, taasisi hizo mbili zilitangaza kuwa zitafanyia utafiti kiwango cha maadili katika taasisi za elimu hapa nchini, na kuzindua vifaa vya elimu kuhusu maadili katika viwango tofauti vya masomo.