Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ametoa wito kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni kuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa taifa hili.
Amesema Wakenya hao wanaweza wakafanya hili kupitia utumaji wa pesa humu nchini na kuunga mkono miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.
Akiwahutubia Wakenya wanaoishi nchini Marekani, Wetang’ula pia amemtaka Balozi wa Kenya nchini humo David Kerich kupanua mitandao yake na kuimarisha hadhi yake Kenya katika diplomasia ya Marekani.
Amemtaka Kerich kufanya hivyo kwa kutambua nyanja za ushirikiano wa pande mbili ambazo zitakuwa zenye manufaa kwa Wakenya.
Spika huyo wa Bunge la Taifa anaongoza ujumbe unaomjumuisha mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi na Seneta wa Makueni Dan Maanzo kuhudhuria Siku ya Taifa ya Maombi itakayofanyika jijini Washington D.C.
Siku hiyo huandaliwa kila mwaka na kuwaleta viongozi mbalimbali kutoka kote duniani, wakiwemo wabunge.