Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi Dijitali, imeibua wasiwasi kuhusu athari za mabadiliko yaliyopendekezwa ya sheria ya nishati kwa uwekaji wa muundombinu wa dijitali kote nchini.
Katibu wa Utangazaji Stephen Isaboke aliwakilisha wizara hiyo mbele ya kamati ya bunge la Seneti kuhusu nishati chini ya uenyekiti wa Seneta Oburu Oginga.
Mabadiliko hayo yanatafuta kukubalia serikali za kaunti kutoza ushuru kwa miundombinu ya umma ya nishati bila hata idhini ya Waziri wa Nishati.
Wizara hiyo ilisema pendekezo hilo lina madhara makubwa kwa miradi ya kitaifa ya uunganishaji na kwamba usimamizi uliogatuliwa utachelewesha utekelezaji wa miradi hiyo na kuongeza gharama ya utekelezaji.
Miradi ya uunganishaji iliyotajwa ni wa uwekaji wa nyaya za intaneti yaani National Optic Fibre Backbone Infrastructure -NOFBI na ule wa uunganishaji umeme mashinani almaarufu Last Mile County Connectivity Project – LMCCP.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliitaka Wizara ya Mawasiliano kuhakikisha kwamba serikali za kaunti zinafaidi kutokana na mapato ya miundombinu ya mawasiliano iliyowekwa kwenye vifaa vya kampuni ya Kenya Power.
Seneta wa Kakamega Dkt. Boni Khalwale kwa upande wake aliunga mkono kuwepo kwa haki akisema viwango vyote viwili vya serikali vinapaswa kufaidika kutokana na mapato ya miundombinu kama hiyo.
Isaboke alitetea mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa mapato akisema kwamba unahakikisha ugavi sawa wa mapato hayo kutumia mfumo wa kitaifa.
Wakili wa Wizara ya Mawasiliano Pauline Kimotho, aliunga mkono usemi wa Katibu huyo akiongeza kwamba changamoto kuu ya kugatua ukusanyaji wa mapato hayo ni ukosefu wa uthabiti katika kaunti.
Maafisa pia walibainisha kuwa pendekezo hilo linakinzana na mifumo ya kitaifa ambayo inasisitiza juu ya uanzishaji wa miundombinu kwa njia iliyoratibiwa na nafuu.
