Kamati ya bunge la taifa kuhusu elimu leo ilikosa kuafikia mapatano na wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma wanaogoma, kuhusu malipo wanayodai serikali.
Kikao cha kamati hiyo leo kilijumuisha waziri wa elimu Julius Migos Ogamba, waziri wa fedha John Mbadi na maafisa wa chama cha wahadhiri kujaribu kusuluhisha mzozo uliopo ili waweze kurejea kazini.
Wahadhiri wanadai malipo ya jumla ya shilingi bilioni 7.9 kutoka kwa serikali waliyokubaliana katika mkataba wa pamoja wa mwaka 2017- 2021.
Serikali kupitia kwa wizara ya fedha ilikuwa tayari imependekeza kwamba pesa zinazodaiwa zilipwe katika awamu mbili, moja mwaka huu wa kifedha na awamu nyingine mwaka ujao wa kifedha.
Wawakilishi wa wahadhiri wakiongozwa na katibu mkuu wa chama chao cha UASU Constantine Wasonga hata hivyo walikataa pendekezo hilo, hata baada ya waziri wa fedha John Mbadi kuongeza malipo ya awamu ya kwanza kutoka bilioni 2.16 hadi bilioni 3.85.
Wasonga alisema kwamba kiwango ambacho wanaweza kukubali ni asilimia 80 ya kiwango wanachodai katika awamu ya kwanza ya malipo na kutokana na hilo, mapatano hayakuafikiwa.
Waziri wa elimu Julius Ogamba alitetea msimamo wa serikali huku akilaumu tume ya mishahara na marupurupu SRC kwa kupotosha serikali kuhusu kiwango halisi cha fedha wanazodai wahadhiri.
Kamati hiyo ya elimu iliwataka mawaziri wa fedha na elimu kujitahidi kusuluhisha mzozo uliopo ili shughuli za masomo zirejelewe katika vyuo vikuu vya umma.
Haya yanajiri wakati ambapo wasimamizi wa vyuo hivyo vikuu wameamua kuvifunga na kuagiza wanafunzi kurejea nyumbani kutokana na mgomo huo wa wahadhiri.
