Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja siku ya Jumanne amepokea timu ya huduma ya kitaifa ya Polisi iliyotwaa ubingwa kwa wanaume na wanawake kwenye mashindano ya kitaifa ya mbio za nyika mwezi uliopita.
Timu ya polisi iliwasilisha mataji iliyonyakua wakati wa mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 19 huku ikitoa wanariadha 11 watakaoiwakilisha Kenya kwa mashindano ya mbio za nyika duniani.
Kanja aliwapongeza wanariadha hao kwa matokeo mazuri na kuipeperusha bendera yao vyema.
Alikariri kujitolea kwa huduma ya kitaifa ya polisi kuwekeza na kutoa kipaumbele kwa michezo ambayo ni chachu muhimu ya kuunganisha maafisa wa polisi.
Wanariadha waliofanya vyema wakati wa mashindano ya kitaifa ya mbio za nyika watashiriki mashindano ya mbio za nyika ulimwenguni mapema Januari mwaka ujao.
Hafla hiyo iliandaliwa katika makao makuu ya NPS, Jogoo House, ambapo wanariadha Daniel Ebenyo Simiu na Mercy Cherono walimkabidhi Kanja vikombe vya timu walivyonyakua mjini Eldoret.