Mwigizaji wa Nollywood Mama Rita Edochie amewafokea wanaovaa vibaya kama wageni waalikwa wa harusi za kanisani. Kulingana naye, harusi za kanisani huashiria usafi na utauwa.
Katika akaunti yake ya Instagram, mama huyo aliandika, “Harusi za kanisani huashiria usafi na utauwa lakini jinsi wanavyohudhuria wakiwa uchi ni jambo la kushangaza.”
Alichapisha video ya mhudhuriaji mmoja wa harusi ya mwigizaji wa Nollywood Ruby Ojiakor iliyofanyika jana ambaye ni mwanamke mwenye mwili mkubwa na matiti yake yanaonekana kabisa.
“Watoto wenu watasema nini wakiona hivi mitandaoni?” alishangaa mama huyo akiendelea kusimulia jinsi mavazi mabaya yameendelea kuwa jambo la kawaida kwenye hafla mbali mbali.
Anahisi kwamba tabia hiyo ambayo sasa imekumbatiwa na wengi ina athari mbaya ikiwa ni pamoja na kudorora kwa maadili ya jamii na kupungua kwa heshima kwa wahusika.
“Ni heri basi utoke kwako ukiwa uchi wa mnyama ndiposa ulimwengu uweze kufahamu kwamba wewe ni mrembo sana na pia wewe ni mwehu”, alisema mama huyo kwa ghadhabu.
Rita ambaye ni shangazi ya Yul Edochie alishauri watu wote wa Nigeria kuchukulia suala la maadili ya kimavazi kwa uzito unaostahili ili kukuza utamaduni wa adabu, unyenyekevu na heshima.
“Ni lazima tutambue athari za tunayochagua kufanya kwa watu binafsi na kwa jamii kwa jumla na kuchukua jukumu la kukuza mazingira chanya na yenye kuinua” alimalizia mama huyo huku akitakia wafuasi wake Jumapili njema.