Mwigizaji wa Nollywood nchini Nigeria Annie Macauley anaonekana kuendela kupiga hatua nzuri maishani hata baada ya kukabiliwa na matatizo yaliyosababisha ndoa yake ya miaka 10 kuvunjika.
Mama huyo wa watoto wawili alikuwa nchini Zimbabwe hivi maajuzi ambako alikuwa amealikwa kuhudhuria hafla ya tuzo za wafanyabiashara.
Annie alichapisha video inayomwonyesha akitambulishwa katika hafla hiyo ambapo alikuwa amevaa vazi la rangi ya samawati kabla ya kuhutubia mkutano huo.
Katika hotuba yake aliahidi kusaidia biashara za waliokuwepo kwa kuzitangaza kwenye mitandao ya kijamii ambapo ana ushawishi mkubwa huku akipongeza wafanyabiashara kwa ustahimilivu.
Alipata fursa ya kutangamana na mke wa Rais wa Zimbabwe Auxillia Mnangagwa ambaye pia alikuwa mmoja wa wageni mashuhuri wa hafla hiyo ambayo mwanzilishi wake ni Primrose January.
Msanii huyo alishukuru waandalizi wa tuzo hizo kwa kumtambua huku akishukuru watu wa Zimbabwe kwa jula kwa makaribisho mema.
“Asante Zimbabwe. Nilikuwa na wakati mwema. Shukrani za dhati kwa Primrose January kwa kuandaa hafla ya hadhi ya juu kwa wanabiashara wa Zimbabwe. Mungu akubariki Malkia” aliandika Annie kwenye Instagram.
Baada ya utengano na mume wake 2Face Idibia, Annie alikabiliwa na msongo wa mawazo uliosababisha apelekwe katika kituo cha kurekebisha na ushauri nasaha.
Alipotoka huko alifuta machapisho yake ya awali kwenye Instagram mwezi machi na kuanza upya kwa kushukuru mashabiki zake kwa kusimama naye. Tangu wakati huo machapisho yake yamekuwa tu kuhusu hatua nzuri anazopiga maishani.