Mwanamuziki wa Marekani Robert Sylvester Kelly maarufu kama R. Kelly anayezuiliwa gerezani anaripotiwa kupatiwa dawa kupita kiasi na kukimbizwa hospitalini baada ya kuzidiwa.
R. Kelly anasema kwamba maisha yake yako hatarini gerezani akidai kwamba wahudumu wa magereza wana njama ya kumuua na walimpa kiwango cha juu cha dawa makusudi.
Wakili Beau B. Brindley amewasilisha kesi mahakamani leo kuhusu tukio hilo akielezea kwamba mteja wake alilazwa hospitali baada ya mmoja wa wahudumu wa gereza kumwelekeza aongeze kiwango cha dawa usiku wa Juni 12, 2025.
Kulingana naye, Kelly aliamka akiwa mnyonge na alipojaribu kusimama alianguka sakafuni akatambaa hadi kwenye mlango wa seli kisha akapoteza fahamu.
Alikimbizwa katika hospitali ya chuo kikuu cha Duke na anadai kusikia mmoja wa wahudumu wa gereza aliyekuwa naye kwenye gari kuelekea hospitalini akilalamika kwamba kisa hicho kingefichua mengi.
Msanii huyo alikaa hospitalini kwa siku mbili na akiwa humo aligundua kwamba kiwango alichopatiwa cha dawa ambazo yeye hutumia kawaida kilitosha kumtoa uhai.
R. Kelly anadai pa kwamba maafisa wa gereza analozuiliwa walimwachisha dawa muhimu ya kupunguza uwezekano wa damu kuganda na hawataki kumruhusu afanyiwe upasuaji uliopendekezwa na daktari wa kuondoa damu iliyoganda miguuni na kwenye maini hatua inayohatarisha maisha yake.
Wakili Brindley anasema Kelly anaamini kwamba atauawa kwenye seli au aachwe huko hadi akufe iwapo hatua haitachukuliwa.
Ombi lake kwa mahakama ni kupatiwa kifungo cha nyumbani kwa muda mfupi, ombi ambalo amewasilisha kwa mara ya tatu sasa akisema kwamba maisha yake yanategemea ombi hilo.