Mwili wa mwigizaji mkongwe wa filamu za Tanzania almaarufu Bongo Movies Hashim Kambi aliyefariki jana, unazikwa leo jijini Dar Es Salaam.
Picha na video zilizosambaa mitandaoni leo zinaonyesha waigizaji na watu wengine maarufu nchini Tanzania wakiwa wamekusanyika katika msikiti wa Maamur Upanga, Dar es Salaam kwa ajili ya mipango ya mazishi.
Mazishi yanapangiwa kufanyika katika makaburi ya Kisutu jijini humo.
Mwili huo uliondolewa kwenye hospitali ya MICO iliyoko Sinza jana jioni huku mke wake aliyeonekana kulemewa na majonzi akiusindikiza hadi makafani ya Masjid Maamur Upanga, Dar es salaam.
Waigizaji wenza wamekuwa wakimwomboleza Hashim kupitia mitandao ya kijamii akiwemo Jackline Wolper ambaye alichapisha picha ya marehemu Hashim ikiwa na mshumaa pembeni na kuandika, “Poleni sana ndugu jamaa na marafiki wote na wanatasnia kwa ujumla. Baba umeniuma sana Umeumwa?? Oooh God”
Rammy Galis naye alichapisha picha aliyopigwa awali na marehemu Kambi na marehemu mwigizaji mwenzao Grace Mapunda huku akimwandikia mwendazake maneno mengi tu ya kumwomboleza.
Galis alikiri kwamba moyo wake umebeba maumivu makubwa sana kwani anahisi amepoteza “Baba” katika tasnia ya uigizaji. Alilalamika akisema kwamba bado alikuwa anendelea kujifunza kusimama bila “Mama” wa tasnia marehemu Grace Mapunda.
“Leo tena naambiwa nijifunze kuishi bila wewe,” aliandika mwigizaji huyo akiahidi kubeba mambo yote waliyomfunza na kwamba atatunza picha yao ya pamoja ambayo ndiyo urithi walimwachia.