Maafisa wa polisi wamewaokoa raia 58 wa Ethiopia, waliokuwa wakizuiliwa katika nyumba moja mtaani Kitengela, wanaoaminika kuwa waathiriwa wa ulanguzi wa binadamu.
Kupitia ukurasa wa X, idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, ilisema ilipokea habari za kijasusi kwamba kundi la raia wa Ethiopia walionekana wakiingia katika nyumba hiyo, na mara moja wakatekeleza operesheni.
Walipoingia katika nyumba hiyo, maafisa hao walisema waliwapata raia hao ambao walionekana kudhoofika kiafya, wanyonge na hawakuwa na vitambulisho vya hapa nchini.
Raia wawili wa Kenya Daniel Nduati Kingoo na Peter Maina Kimemia pia walipatikana katika nyumba hiyo, na walikamatwa na maafisa wa polisi
Uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa waathiriwa hao waliwasilishwa katika nyumba hiyo siku tatu zilizopita, wakisubiri kusafirishwa hadi Afrika kusini.
Waathiriwa 28 walipelekwa katika kituo cha polisi cha Kitengela, 30 katika kituo cha polisi cha Isinya, huku wakenya hao wawili wakizuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.