Mudavadi atoa wito wa uchaguzi wa amani 2027

Alizungumza katika uzinduzi wa mpango unaojulikana kama “Roadmap to a Violence-Free 2027 General Election, Uchaguzi Bila Noma.”

Marion Bosire
2 Min Read

Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, amewataka Wakenya na viongozi wa kisiasa kuweka mbele amani na utulivu wakati nchi ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mpango wa Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 Usio na Vurugu, unaojulikana kama “Roadmap to a Violence-Free 2027 General Election, Uchaguzi Bila Noma,” Mudavadi aliwataka viongozi wa kisiasa, taasisi za serikali, jumuiya za kidini, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wananchi kulinda amani ya Kenya.

Alisema uchaguzi wa amani sio muhimu tu kwa utulivu wa kisiasa, bali pia una manufaa makubwa kiuchumi, ikiwemo kuongeza imani ya wawekezaji, kulinda riziki za wananchi na kutoa fursa kwa vijana kujenga maisha yao ya baadaye.

“Amani sio suala la kisiasa pekee, ina thamani halisi kiuchumi,” alisema Mudavadi, akionya kuwa ukosefu wa utulivu huathiri zaidi Wakenya wa kawaida.

Aliwahimiza hasa vijana kushiriki mijadala ya kisiasa, kuuliza viongozi maswali na kudai uwajibikaji bila kuruhusu tofauti za kisiasa au mitandao ya kijamii kuwageuza Wakenya wenzao kuwa maadui.

Mudavadi pia alisisitiza umuhimu wa kuheshimu taasisi na kutumia lugha ya kisiasa yenye uwajibikaji, akisema ushindani wa kisiasa unapaswa kuwa wa amani na ujumbe wa viongozi uunganishe badala ya kuchochea Wakenya.

Alisema ushindi mkuu baada ya uchaguzi wa 2027 unapaswa kuwa wa Kenya, bila kujali matokeo ya kisiasa.

Share This Article