Mswada wa Uchumi wa Ubunifu wawasilishwa bungeni

Unalenga kuweka mfumo wa kisheria na kitaasisi wa kusaidia ukuaji, maendeleo na uendelevu wa uchumi wa ubunifu nchini Kenya

Marion Bosire
2 Min Read
Dan Wanyama, Mwenyekiti wa Kamati ya Idara ya Michezo na Utamaduni bungeni

Mswada wa Uchumi wa Ubunifu wa mwaka 2026, unaolenga kuweka mfumo wa kisheria na kitaasisi wa kusaidia ukuaji, maendeleo na uendelevu wa uchumi wa ubunifu nchini Kenya, umewasilishwa katika Bunge la Kitaifa.

Mswada huo, unaodhaminiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Idara ya Michezo na Utamaduni, Dan Wanyama, unalenga kuunganisha sekta ya uchumi wa ubunifu na kurahisisha majukumu ya taasisi zinazohusika na uhamasishaji, maendeleo na udhibiti wake.

Iwapo utapitishwa kuwa sheria, Mswada utaanzisha Tume ya Kenya ya Sauti, Picha na Sinema, Mamlaka ya Udhibiti wa Sauti na Picha ya Kenya na Shule ya Kenya ya Filamu na Sanaa za Ubunifu, huku ukitenganisha wazi majukumu ya kukuza sekta na yale ya kuidhibiti.

Mswada huo pia unapendekeza kuandaliwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Sekta za Ubunifu ili kutoa mfumo wa kimkakati wa kukuza sekta hiyo.

Mfumo huo utalenga kuimarisha maendeleo ya ujuzi kupitia Shule ya Kenya ya Filamu na Sanaa za Ubunifu, pamoja na kuweka muundo wa wazi zaidi wa kitaasisi kwa sekta hiyo.

Ili kuimarisha usaidizi kwa wabunifu, Mswada unapendekeza maendeleo ya miundombinu, ufadhili wa utafiti na ubunifu, kuanzishwa kwa vituo na nguzo za ubunifu, na kuunganisha zaidi sekta za ubunifu na taasisi za elimu na masoko ya mitaji.

Aidha, unapendekeza kuanzishwa kwa Hazina ya Maendeleo ya Sekta ya Ubunifu na kukuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuhamasisha uwekezaji na kusaidia ukuaji wa biashara za ubunifu.

Share This Article