Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu ameridhia ombi la Makamu wake Dkt. Emmanuel John Nchimbi kujiuzulu wadhifa huo.
Kwenye taarifa, Suluhu amesema taratibu za kumtafuta mrithi zitafuatwa kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 25 Agosti, 2026, amepokea barua ya ombi la kujiuzulu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuanzia tarehe 04 Septemba, 2026. Mheshimiwa Rais ameridhia ombi hilo,” alisema Suluhu kupitia kwenye taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka.
“Taratibu za kikatiba za kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwingine zitachukuliwa,” iliongeza taarifa hiyo fupi yenye aya mbili.
Awali, kwenye taarifa, Dkt. Nchimbi alidokeza kuwa amemwandikia Rais Suluhu barua ya kujiuzulu kwake kuanzia Septemba 04 mwaka huu, ambayo itakuwa mwaka mmoja tangu ashike hatamu za wadhifa huo.
“Agosti 27 mwaka uliopita, nilimuahidi Rais Dkt. Samia Suluhu kuwa nitatekeleza majukumu yangu kwa uadilifu na uwezo wangu. Pia nilimhakikishia kuwa siku nitakayohisi kuwa siwezi kutekeleza kazi yangu jinsi nilivyoahidi, nitamuarifu. Nimemjuza leo kuwa muda wangu wa kutimiza ahadi yangu umetimia, na ningependa kujiuzulu,” alisema Dkt. Nchimbi.
Makamu huyo wa Rais aidha alimshukuru Rais kwa kuwa na imani naye na pia kuwashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono kwa wakati aliohudumu.
Nchimbi anakuwa Makamu Rais wa kwanza kujiuzulu wadhifa huo katika historia ya nchi hiyo.