Rais William Ruto leo Jumanne aliungana na viongozi wengine kutoka barani Afrika mjini Dar es Salaam, Tanzania, kwa uzinduzi wa mpango unaolenga kuhakikisha watu milioni 300 barani humo wanaunganishiwa umeme katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi wa Afrika pia uliwaleta pamoja viongozi kutoka sekta za kifedha na wahisani duniani waliohudhuria uzinduzi huo unaokusudia kuharakisha usambazaji wa umeme barani Afrika.
Ukiwa umeitwa “Misheni 300,” mpango huo unalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme nafuu na endelevu kwa watu zaidi ya milioni 600 wasiokuwa na umeme kwa sasa barani humo kufikia mwaka 2030.
“Mkutano huu unazidi nishati; unahusu kuziwezesha familia, kuinua mamilioni kutoka kwenye umaskini, kutoa matumaini na fursa kwa vijana,” alisema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa waliokuwepo walikuwa Wakuu kadha Nchi na Serikali, miongoni mwao Rais Mohamed Ould Ghazaouani wa Mauritania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU.
Washirika wakuu kwenye mpango huo wanajumuisha Kundi la Benki ya Dunia, Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Rockefeller Foundation na AU.
Benki ya Dunia inatoa kati ya dola bilioni 30-40 kwenye mpango huo huku AfDB ikiwekeza dola bilioni 18 katika kipindi hicho cha miaka mitano.
Pembezoni mwa mkutano huo, Rais Ruto alifanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed na kuzungumzia upunguzaji wa mgogoro unaozidi kushuhudiwa mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC.