Haikuwa Ebola, asema Katibu Muthoni kuhusu kisa cha Kiambu

Serikali inasema imeweka mikakati ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo uliotokea katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mary Muthoni - Katibu katika Wizara ya Afya

Ni afueni baada ya serikali kubaini kuwa raia wa Uturuki aliyedaiwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ebola katika hospitali ya AAR, kaunti ya Kiambu siku chache zilizopita amebainika kutoambukizwa ugonjwa huo.

Hofu ilitanda katika mitandao ya kijamii baada ya taarifa kuibuka kuwa raia huyo alifikishwa hospitalini hapo akionyesha dalili za ugonjwa huo.

Hata hivyo, Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni amesema uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa raia huyo hakuambukizwa virusi hatari vya ugonjwa wa Ebola.

“Kufuatia taarifa ya kisa kilichoshukiwa cha Ebola kutoka Hospitali ya AAR katika kaunti ya Kiambu, Wizara ya Afya, kwa ushirikiano na Idara ya Afya ya Kaunti hiyo na wataalam husika wa afya ya umma, iliweka taratibu za haraka za uangalizi na mwitikio. Mgonjwa huyo alifanyiwa uchunguzi wa kitabibu, hatua zifaazo za uzuiaji na udhibiti kutekelezwa, na sampuli za maabara kukusanywa na kuwasilishwa ili kupimwa,” alisema Katibu Muthoni kwenye taarifa.

“Wizara ingependa kuuarifu umma kuwa uchunguzi wa maabara umethibitisha kuwa mgonjwa huyo hakupatikana na ugonjwa wa virusi vya Ebola.”

Muthoni amesema serikali imeweka mikakati madhubuti kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda.

“Tungependa kuwahakikishia Wakenya kuwa kwa sasa hakuna kisa cha Ebola kilichothibitishwa kikihusishwa na ripoti hii. Wizara inaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali za kaunti, vituo vya afya, maeneo ya kuingia nchini, na washirika wa kitaifa na kimataifa kuimarisha uwezo wa maandalizi na mwitikio dhidi ya Ebola na matishio mengine ya afya ya umma.”

Kadhalika amewataka Wakenya kutafuta habari kutoka kwa vyanzo vya kuaminika.

Share This Article