Tanzania na Angola kuimarisha ushirikiano wa kibiashara

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mahmoud Kombo akiwa na António Duarte Gomes ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi ya TEGMA-SU LDA ya Angola  

Mataifa ya Tanzania na Angola yamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya biashara kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinakazokidhi mahitaji ya watu, soko la kikanda na kimataifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo wakati alipokutana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini Angola ukiongozwa na António Duarte Gomes ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi ya TEGMA-SU LDA ya Angola.

Aidha, katika mazungumzo hayo, Kombo amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Angola katika kuongeza uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa kufuatia uboreshaji wa miundombinu unaoendelea kutokea ushoroba wa Robito, kupitia Zambia hadi Bandari ya Dar es Salaam kwa reli ya TAZARA.

Uboreshaji wa miundombinu hiyo utarahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu kutoka Bahari ya Atlantiki kuelekea Bahari ya Hindi.

Kombo pia amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Angola kuwekeza katika usafiri wa anga ili kuwa na usafiri wa moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili utakaorahisisha shughuli za usafirishaji.

Waziri huyo pia alitumia fursa hiyo kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara ambapo ameeleza kuwa kwa upande wa Zanzibar, kuna fursa nyingi za uwekezaji katika utalii. Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana katika sekta ya kilimo pamoja na madini.

Kwa upande wake, Gomes alimshukuru Kombo kwa ushirikiano wanaoendelea kuupata.

Ukiwa nchini Tanzania, ujumbe huo utatembelea eneo ambalo Baba wa Taifa wa Angola Hayati António Agostinho Neto aliwahi kuishi enzi za harakati za ukombozi wa taifa hilo na Afrika kwa ujumla.

Tanzania na  Angola zimekuwa zikishirikiana tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na hata baada ya kupatikana kwa uhuru.

Kwa misingi hiyo, ushirikiano wa mataifa hayo umeendelea kuimarika katika masuala ya kisiasa, kijamii na hata kiuchumi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *