Wanahabari katika kaunti ya Turkana wameandamana mjini Lodwar, wakiwanyoshea kidole cha lawama maafisa wakuu katika serikali ya kaunti hiyo kwa kile wanachokitaja kuwa ongezeko la kutishiwa maisha na kunyimwa uhuru wa kutekeleza majukumu yao ya wanahabari kwa mujibu wa sheria.
Wiki moja iliyopita, wanahabari wa Turkana walipeperusha taarifa kuhusu ubomozi wa darasa la chekechea katika shule ya msingi ya Kapoo, darasa lililojengwa na mcheshi Erick Omondi.
Zoezi la ubomozi lilidaiwa kutekelezwa na maafisa wakuu wa kaunti ya Turkana wakiongozwa na Waziri wa Elimu wa kaunti ya Turkana Wiljustus Lopeyok.
Inasemekana taarifa hiyo haikuwafurahisha viongozi hao na wameanza kutishia wanahabari kwa kuwatumia jumbe pamoja na kupiga simu, huku wale waliohojiwa kwa taarifa hiyo pia wakidai maisha yao yamo hatarini.
Kufikia sasa, baadhi ya wanahabari husika wameanza kutoroka huku wengine wakilazimika kuishi kwa marafiki.