Waziri wa Ardhi Alice Wahome ameahidi kuongoza kampeni ya kutwaa ardhi yote ya umma iliyonyakuliwa kote nchini, akikariri kuwa uvamizi na umiliki haramu wa ardhi hautavumiliwa.
Akizungumza alipozuru sajili ya ardhi kaunti ya Kiambu, Wahome alidokeza kuwa wizara yake kwa sasa inajumlisha rekodi ya ardhi ya umma iliyonunuliwa kwa njia haramu ili kuitwaa, kipaumbele kikiwa ni ardhi iliyokusudiwa kuwa ya shule katika kaunti za Nairobi na Mombasa.
Waziri huyo aliwataka wale wanaomiliki ardhi kinyume cha sheria, kusalimisha hatimiliki au wachukuliwe hatua za kisheria.
“Ardhi ya shule ya upili ya Nyali imenyakuliwa na watu wamejenga kwenye ardhi hiyo. Lakini tutachukua ardhi hiyo,” alisema Waziri huyo.
“Wale ambao wameshikilia hatimiliki ya ardhi ya shule ya upili ya Nyali, sikilizeni, naja Mombasa kutwaa ardhi hiyo. Pia tunajizatiti kutwaa ardhi inayomilikiwa na shule ya msingi ya Lavington jijini Nairobi,” alionya Wahome.
Alitoa wito kwa wakuu wa shule kushirikiana na afisi yake badala ya kufanikisha usajili wa ardhi yao, huku anapojitahidi kutatua mizozo ya umiliki wa ardhi inayomilikiwa na taasisi mbalimbali.
Aidha, alisema juhudi zinatekelezwa kuzipa mianya katika Wizara ya Ardhi kupitia uwekaji rekodi kidijitali.
“Mfumo wa dijitali unalenga kuimarisha uwazi, ufanisi na kuwezesha upatikanaji wa rekodi za ardhi kupitia mtandao na ubadilishanaji wa umiliki wa ardhi,’ alidokeza Wahome.