Kundi moja la kupigania maongozi bora katika kaunti ya Embu limemtetea Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi na kumtaka Rais William Ruto kuunda Tume ya Uchunguzi kuchunguza visa vya hivi karibuni vya utekaji nyara wa vijana nchini.
Wakiwahutubia wanahabari mjini Embu, wanachama vijana wa kundi linalofahamika kama “Good Governance Lobby Group” wamewashutumu viongozi kutoka Bonde la Ufa na Magharibi mwa nchi ambao wamemtaka Muturi kujiuzulu.
Kulingana na kundi hilo, Muturi ameelezea wasiwasi walio nao Wakenya wengi na kuitaka serikali kuchukulia kauli zake kwa dhati.
Vijana hao pia wametangaza mipango ya kuzuru maeneo mbalimbali ya nchi kushinikiza kukomeshwa kwa visa vya utekaji na uchunguzi madhubuti kufanywa ili kuhakikisha wahusika wa visa hivyo wanawajibishwa kisheria.