Wakazi Mayungu walalamikia uhaba wa maji

Wametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watoa huduma za maji.

Marion Bosire
2 Min Read

Wakazi na wamiliki wa biashara katika eneo la Mayungu, Kaunti Ndogo ya Malindi, kaunti ya Kilifi wamelalamikia uhaba uliokithiri wa maji.

Wametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watoa huduma za maji kwa kile wanachokitaja kuwa uzembe na kushindwa kutoa huduma za kuaminika.

Khairunisa Suleiman, mkazi wa Mayungu, anasema ameishi hapo tangu mwaka 2023 na amekuwa akishuhudia ukosefu wa maji mara kwa mara, hasa wakati wa msimu wa kilele wa utalii kati ya mwezi Novemba na Januari.

Hali hiyo anasema ilizidi kuwa mbaya mwaka uliopita, huku mabomba yakikauka katika nyumba, hoteli na biashara zilizoko Mayungu, likiwemo Soko la Mayungu.

Wakazi hao wanasema wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara na Kampuni ya Maji na Majitaka ya Malindi, MAWASCO, lakini wamekuwa wakipewa maelezo mbalimbali.

Maelezo hayo yanajumuisha uzalishaji wa kiwango cha chini cha maji kutoka kwa Wakala wa Maendeleo ya Huduma za Maji wa Pwani, CWWDA, visima kuzibwa kutokana na tope na kukatwa kwa umeme kwa sababu ya bili ambazo hazijalipwa.

Mkazi mwingine, Renson Kenga Mayungu, alisema tatizo la maji linatishia uchumi wa utalii wa mji huo.

Mkazi wa tatu, Samuel Ndonya, alisema baadhi ya maboma yamelalamikia kutumia maji yenye chumvi, huku wale wenye uwezo wa kifedha wakilazimika kununua maji kutoka kwa wauzaji binafsi.

Alihimiza serikali ya kitaifa, ya kaunti na viongozi wa eneo hilo kuingilia kati haraka na kurejesha huduma za maji za kuaminika katika eneo la Mayungu.

Wakazi sasa wanatishia kupeleka MAWASCO na Coast Water mahakamani, wakizishutumu kampuni hizo kwa uzembe na kudai majibu kuhusu sababu ya kuendelea kwa uhaba huo wa maji.

Wanataka pia uchunguzi ufanywe kuhusu kile wanachoshuku kuwa huenda kikawa njama kati ya watoa huduma za maji na wauzaji binafsi.

Aidha, wakazi wamehoji namna usambazaji wa maji unapangwa, wakidai kuwa maji mengi zaidi yanaelekezwa Mombasa huku jamii katika kaunti ya Kilifi zikiendelea kukabiliwa na uhaba.

Share This Article