Polisi wanaohusika vifo vinavyotokea korokoroni kuwajibishwa

Kumekuwa na visa kadhaa vilivyoripotiwa vya washukiwa kufariki wakiwa katika vituo vya polisi nchini.

Martin Mwanje
2 Min Read
Douglas Kanja - Inspekta Mkuu wa Polisi

Polisi yeyote atakayebainika kuhusika katika vifo vya washukiwa vinavyotokea wakati wakizuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini atawajibishwa kwa mujibu wa sheria. 

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja anasema uchunguzi madhubuti utafanywa punde baada ya kifo chochote cha mshukiwa kuripotiwa kwa lengo la kubaini chanzo chake.

“Pale mshukiwa anapofariki akiwa katika korokoro ya polisi, uchunguzi kamili utaanzishwa bila kukawia kwa mujibu wa Katiba, sheria husika, na taratibu zilizowekwa za upelelezi. Mchakato wa sheria utazingatiwa katika kila hatua, ikiwa ni pamoja na hatua za kusimamishwa kazi inapohitajika,” alisema Kanja kwenye taarifa iliyotumwa na msemaji wa Huduma ya Taifa ya Polisi, Muchiri Nyaga.

“Ikiwa polisi yeyote atabainika kuhusika katika kifo chochote wakati wa uchunguzi kama huo, hatua za haraka na madhubuti zitachukuliwa. Afisa anayehusika atawajibishwa kikamilifu chini ya sheria na kupitia taratibu za ndani zilizowekwa za Huduma.”

Kanja aliyasema hayo wakati ambapo visa kadhaa vya washukiwa kufariki wakiwa katika korokoro za polisi vimeripotiwa nchini.

Cha hivi karibuni zaidi ni kile cha mfanyabiashara Gedion Makau aliyepatikana amefariki katika kituo cha polisi cha Kilungu katika kaunti ya Makueni.

Aidha, kifo cha mwalimu Albert Ojwang katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi kiligonga vichwa vya habari na maafisa kadhaa wa polisi kukamatwa.

Kesi ya kuitendea familia ya marehemu Ojwang haki bado inaendelea.

 

Share This Article