Miano aongoza maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani ya Umoja wa Mataifa

Sherehe hizo zilizofanyika katika Chuo Kikuu cha Eldoret ziliangazia utofauti wa sekta ya utalii nchini Kenya.

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Rebecca Miano, jana aliongoza Kenya katika kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2026.

Alifanya hivyo jijini Eldoret, ambalo ni mwenyeji wa kilele cha sherehe za Wiki ya Utalii nchini Kenya zilizodumu wiki moja.

Sherehe hizo zilizofanyika katika Chuo Kikuu cha Eldoret ziliangazia utofauti wa sekta ya utalii nchini Kenya, huku eneo la North Rift likiwa kitovu cha maadhimisho hayo.

Eneo hilo liliangazia urithi wake mkubwa wa michezo, tamaduni mbalimbali, mandhari ya kuvutia na ongezeko la bidhaa na huduma za utalii.

Hafla hiyo iliadhimisha nguzo muhimu za utalii nchini Kenya, zikiwemo utamaduni, michezo, wanyamapori, vyakula, ubunifu na jamii zinazozipa vivutio vya utalii upekee wake.

Jukumu linaloongezeka la ubunifu wa kidijitali na Akili Unde, AI, katika sekta ya utalii pia lilipewa kipaumbele. Kenya inachunguza teknolojia hizi kama nyenzo za kutangaza maeneo ya utalii, kuwashirikisha wageni na kuboresha uzoefu wa watalii.

Sherehe hizo pia zilisisitiza mchango wa utalii kwa jamii na biashara na fursa zinazotokana na kuunganisha maeneo ya utalii na wageni kutoka Kenya na duniani kote.

Uteuzi wa Eldoret kuwa mwenyeji ni ishara ya umuhimu unaokua wa North Rift katika utalii wa Kenya, hasa kupitia utambulisho wake wa michezo, urithi wa kitamaduni na mazingira ya kipekee.

Sherehe hizo zilinatilia mkazo ukweli kwamba utalii hauishii kwenye maeneo ya kutembelea pekee, bali unahusisha watu, uzoefu, biashara, urithi na fursa.

Share This Article