Ommy Dimpoz afafanua tukio lake na maafisa wa TRA

Lilihusisha maafisa wa TRA, ambapo anasisitiza kuwa hakuwa na nia ya kuwazuia maafisa hao kutekeleza majukumu yao.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Tanzania, Omary Nyembo maarufu kama Ommy Dimpoz, amefafanua kuhusu tukio lililotokea usiku wa kuamkia Septemba 26, 2026.

Tukio hilo lilihusisha maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania,TRA, ambapo anasisitiza kuwa hakuwahi kuwa na nia ya kuwazuia maafisa hao kutekeleza majukumu yao.

Kupitia ujumbe kwenye akaunti yake ya Instagram, Ommy Dimpoz amesema amekuwa raia mtiifu wa Tanzania muda wote wa maisha yake na kwamba amekuwa akishirikiana na maafisa wa Serikali pale anapohitajika kufanya hivyo.

“Ndugu zangu, najivunia kwamba nimekuwa raia mtiifu kwa muda wote wa maisha yangu, sikuwahi, sio, na sitegemei kuwa mvunja sheria za nchi kwa kukusudia na miongoni mwa mambo ambayo siwezi kamwe kuyafanya ni kuzuia watendaji wa Serikali kutimiza wajibu wao,” aliandika.

Ommy Dimpoz ameomba radhi kwa yeyote ambaye huenda alikwazika au kupata tafsiri isiyofurahisha kutokana na tukio hilo, huku akiahidi kujitahidi kuepuka kujikuta katika mazingira kama hayo siku zijazo.

“Niwaombe radhi wote waliokwazika na jambo lile na kuwaomba kuliondoa vichwani mwao, sikukusudia liwe jinsi lilivyotokea,” amesema, huku akiwataka Wananchi wenzake kutoa ushirikiano kwa Watumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao.

Usiku wa Septemba 25, 2026, Msanii huyo alikwazana na maafisa wa TRA kutokana na madai kwamba gari lake halikuwa limetimiza masharti ya kodi.

Share This Article