Murkomen: Kenya na Uganda zinafurahia ushirikiano wa pamoja wa kitamaduni

Murkomen alithibitisha kuwa Kenya imejitolea kuwa balozi wa amani, usalama na ufanisi wa pamoja.

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ahudhuria sherehe ya kutoa shukrani ya shule ya Upili ya Amanang nchini Uganda.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema Kenya na Uganda zinafurahia ushrikiano wa pamoja wa Kijamii, Kitamaduni na Kiuchumi.

Akizungumza Ijumaa alipohudhuria sherehe ya kutoa shukrani ya shule ya upili ya Amanang  katika mkoa wa Bukwo nchini Uganda, Murkomen alidokeza kuwa Kenya itaendelea kuunga mkono usafiri huru wa raia, ili kufanikisha wananchi wa mataifa hayo mawili kufanya kazi, kuishi na kushiriki biashara pamoja, kuambatana na makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tulihimiza pia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa usalama mipakani, kukabiliana na wizi wa mifugo, ujangili na shughuli zingine za kiuhalifu,” alisema Murkomen.

Kulingana na Murkomen, maafisa wa usalama kutoka Pokot Magharibi na wenzao kutoka maeneo ya Uganda, wameagizwa kushirikiana pamoja kuhakikisha amani ya kudumu kwa jamii za pande zote mbili za mpakani.

“Hatutawakubalia wahalifu kutekeleza maovu katika nchi moja na kutafuta hifadhi katika nchi nyingine,” alisema Murkomen.

Murkomen alithibitisha kuwa Kenya imejitolea kuwa balozi wa amani, usalama na ufanisi wa pamoja.

Kwenye sherehe hiyo, waziri huyo alikuwa ameandamana na Seneta wa Trans Nzoia Allan Chesang, mbunge wa Endebess Robert Pukose, mwakilishi mwanamke Lilian Siyoi, mbunge wa Kiminini Kakai Bisau,na balozi wa Kenya nchini Uganda Ababu Namwamba, miongoni mwa viongozi wengine.

Upande wa Uganda uliwakilishwa na Kapyagon Brian Besta, Chelangat Evelyn Tete (Mwakilishi mwanamke), Chesol Tom (mwenyekiti wa wilaya ya Bukwo), na Chelimo Vincent (Mwenyekiti wa wilaya ya Kapchorwa), miongoni mwa wengine.

Share This Article