Mwimbaji wa Uganda Kabaya, ambaye jina lake halisi ni Joseph Bwogi, amekanusha madai ya Polisi wa Uganda kwamba alikamatwa katika operesheni iliyolenga watumizi wa dawa za kulevya.
Amesisitiza kuwa kukamatwa kwake kulichochewa na siasa.
Haya yanajiri baada ya mwanamuziki huyo wa zamani wa Firebase Crew na mfuasi wa wazi wa Bobi Wine kudai kuwa alikamatwa na polisi na kupigwa kikatili, hali iliyosababisha apoteze meno manne.
Baadaye aliachiliwa kwa dhamana ya polisi na kurejea nyumbani kuungana na familia yake huku akitafuta matibabu.
Akizungumzia madai hayo, msemaji wa Polisi jijini Kampala, Racheal Kawala, alithibitisha kuwa Kabaya alikamatwa katika operesheni ya polisi.
Kwa mujibu wa Kawala, mwanamuziki huyo alikamatwa kwa madai ya kutumia dawa za kulevya na baadaye akaachiliwa kwa dhamana ya polisi.
Aliongeza kuwa ikiwa Kabaya anaamini alipigwa na maafisa wa polisi, anapaswa kuwasilisha malalamiko rasmi ili uchunguzi ufanyike.
Kabaya amepinga vikali maelezo ya polisi, akisisitiza kwamba hakuhusika na matumizi ya dawa za kulevya wala hakukamatwa katika msako wowote.
Mwimbaji huyo anadai kuwa polisi walimzuia nje ya nyumba yake baada ya kufunga njia yake kwa gari la doria la polisi, kabla ya kumtambua kama “rafiki wa Bobi Wine” kisha kumpiga vibaya na kusababisha ang’oke meno manne.
Kabaya amesema sasa analenga kutafuta haki, akitaka maafisa anaowatuhumu kwa kumshambulia wawajibishwe.