Mwana TikTok atoweka Uganda na kusababisha wasiwasi

Innomighty Media, anaripotiwa kutoweka muda mfupi baada ya kuripoti kuhusu tamasha ya mwimbaji wa nyimbo za Injili, Lillian Nabaasa.

Marion Bosire
1 Min Read

Jamaa mmoja anayejihusisha na uundaji maudhui mitandaoni nchini Uganda alitoweka hali ambayo imesababisha hofu na wasiwasi kati ya wenzake wa mtandao wa kijamii wa TikTok, nchini humo.

Marafiki za jamaa anayeendesha akaunti iitwayo Innomighty Media, wanaelezea kwamba alitoweka muda mfupi baada ya kuripoti tamasha ya mwimbaji wa nyimbo za Injili, Lillian Nabaasa, katika Hoteli ya Serena Kampala jana usiku.

Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa, TikToker huyo alidaiwa kuzuiwa na kundi la wanaume waliovalia sare za kijeshi na kufunika nyuso zao.

Watu hao walionekana wakimbeba kwa nguvu na kulazimishwa kuingia kwenye gari jeupe lenye namba za usajili UAV 949A, ambalo linadaiwa kuondoka kwa kasi katika eneo hilo.

Tukio hilo la kushtua limezua hofu miongoni mwa wenzake na wafuasi wake, huku maswali yakiongezeka kuhusu alipo na nani huenda akahusika na kile kinachodaiwa kuwa kukamatwa kwake.

Hata hivyo, maelezo kuhusu tukio hilo bado hayajawekwa wazi, na hakuna uthibitisho rasmi unaoeleza kilichotokea.

Sasa macho yote yanaelekezwa kwa polisi na vyombo vya usalama ili kufafanua mazingira yaliyosababisha kutoweka kwake, pamoja na kutoa taarifa kuhusu alipo.

Share This Article