Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi ametoa wito kwa wakazi wa Siaya kumuunga mkono Rais William Ruto kugombea muhula wa pili katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Amesema utawala wa sasa umeanzisha mipango kochokocho ya maendeleo katika eneo hilo kwa muda ambao umekuwa madarakani.
“Tuna miradi katika nchi hii ambayo kamwe hungeiona kama isingekuwa kwa sababu ya uongozi wa Rais William Ruto,” alisema Wandayi aliyehudumu kama mbunge wa Ugunja kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri.
“Hatuna majuto. Lazima tuje pamoja na kumuunga mkono Rais kupata muhula wa pili. Kuanzia wiki hii, tunaenda kuwa makini zaidi kwamba lazima mdhihirishe mchango wenu.”
Wandayi pia alitoa wito wa amani na uthabiti wa kisiasa nchini akitaja vyote hivyo kuwa vichocheo muhimu vya maendeleo.
Pia ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kujiandikisha kwa wingi kama wapiga kura kwani hatua hiyo itaimarisha ushawishi wa eneo hilo katika ngazi ya kitaifa.
“Kwenda mbele, lazima tujue kwamba idadi yetu au idadi ya kura yetu, itaamua sisi kama watu wa Siaya tunakaa katika meza ya taifa,” alisema Wandayi.
Alitoa changamoto kwa wanasiasa wanaotafuta nafasi za uongozi katika kaunti hiyo kuonyesha dhamira yao kwa uandikishaji wa wapiga kura, akionya kuwa uungwaji mkono wa kisiasa utalingana na mchango wao kwa uandikishaji wa idadi ya wapiga kura.
“Hakutakuwa na cha bwerere. Ikiwa unatutaka kukuunga mkono katika kaunti hii, kwanza kabisa, dhihirisha kuwa unachangia ipasavyo uandikishaji wa wapiga kura,” aliongeza Wandayi akisema takwimu kamwe huwa hazidanganyi.
Katibu katika Wizara ya Habari na Uchumi wa Dijitali Stephen Isaboke, aliyekuwapo, alizungumzia ajenda ya dijitali ya serikali, akitoa mfano wa vituo vya dijitali vilivyoanzishwa katika maeneo ya Rarieda na Bondo.
Alivitaja kuwa ishara ya wazi ya dhamira ya serikali kuwawezesha vijana.
Isaboke alisema ajenda ya dijitali ya serikali ni sehemu ya ajenda ya maendeleo ya Rais Ruto na inadhamiria kupanua fursa za kidijitali kwa vijana nchini.
“Tunamfanyia kazi Mheshimiwa Rais, Dkt. William Samoei Ruto. Ameweka mipango, na moja ya mipango hiyo ni ajenda ya dijitali,” alisema Isaboke.
Aliongeza kuwa vituo vilivyoanzishwa katika maeneo ya Rarieda na Bondo vinawahudumia mamia ya vijana siyo tu kutoka eneo hilo bali kutoka maeneo mengine.