Serikali yatoa shilingi bilioni 3.3 za wanafunzi wa vyuo vikuu

Martin Mwanje
2 Min Read
Julius Ogamba - Waziri wa Elimu

Ni afueni kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili katika vyuo vikuu baada ya serikali kutoa jumla ya shilingi bilioni 3.32 za kufadhili masomo yao. 

Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba anasema fedha hizo zilisambazwa kufikia Januari 31 mwaka huu kwa ajili ya mwaka wa masomo wa 2024/2025.

“Fedha zilizosambazwa kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB), zinajumuisha fedha za wanafunzi kujikimu kimaisha. Mikopo ya kujikimu, ambayo ni nguzo muhimu ya kukuza maslahi ya wanafunzi, ni ya kiwango cha shilingi 40,000 hadi 60,000 kwa kila mwanafunzi,” alisema Waziri Ogamba.

“Fedha zilizosambazwa hivi punde ni sehemu ya fedha ambazo tayari zilikuwa zimetengwa mwezi Julai mwaka 2024, katika muktadha wa mpangokazi wa bajeti na matumizi ya mwaka wa fedha wa sasa.”

Fedha hizo zimetolewa wakati ambapo wanafunzi wa vyuo vikuu wamekuwa wakiishinikiza serikali kutoa fedha za kufadhili masomo yao, wakilalama kuwa hatua ya serikali kukawia kutoa fedha hizo imekuwa mwiba kwa juhudi zao za kupata kisomo.

Baadhi yao walihofia mamlaka ya vyuo vikuu kuwazuia kufanya mitihani.

Jana Jumatatu, usimamizi wa HELB uliashiria kuwa utatumia mfumo wa zamani kuwasambazia wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili katika vyuo vikuu fedha za kufadhili masomo yao ikisubiri uamuzi wa mahakama juu ya rufaa iliyokatwa na serikali.

Rufaa hiyo ilikatwa baada ya mahakama kuagiza kuwa mfumo huo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu usitishwe hadi pale kesi iliyowasilishwa kuupinga isikizwe na kuamuliwa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *