Mgonjwa mkongwe zaidi wa saratani aenziwa Meru

Siku hii ilisadifiana na kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ya mgonjwa huyo aitwaye M'Mugambi M'Marete wa umri wa miaka 104.

Marion Bosire
1 Min Read

Ulimwengu ulipokuwa ukiadhimisha siku ya saratani, wahudumu wa hospitali ya Meru hospice waliamua kuadhimisha siku hiyo kwa kumsherehekea mgonjwa wao mkongwe zaidi wa saratani.

Mgonjwa huyo kwa jina M’Mugambi M’Marete wa umri wa miaka 104 alibebwa kutoka nyumbani kwake hadi hospitalini humo na gari la hospitali kusherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa anapotimiza umri wa miaka 104.

Aligunduliwa kuwa na saratani mwaka 2017 na tayari ilikuwa imefikia kiwango cha nne na kutokana na umri wake waliamua tu kumtunza na kumpa huduma za kumpunguzia maumivu.

Kulingana na msimamizi wa hospitali hiyo ya Meru hospice Gladys Mucee, taasisi hiyo ya afya imekuwepo kwa miaka 20 sasa na wameweza kuhudumia wagonjwa zaidi ya elfu 5 wa saratani wakazi wa kaunti ya Meru na wa kaunti nyingine jirani.

Gladys alisema kwa wakati huu wanahudumia wagonjwa 502 wa saratani, mgonjwa wa umri mdogo zaidi akiwa mtoto wa mwaka mmoja na mkongwe zaidi akiwa M’Mugambi wa umri wa miaka 104.

Siku ya saratani ulimwenguni huadhimishwa Februari 4 kila mwaka na ilianzishwa mwaka 2000 katika kongamano la ulimwengu la saratani jijini Paris nchini Ufaransa.

Lengo kuu ni kutoa uhamasisho kuhusu maradhi hayo na kuhimiza uzuiaji, ugunduzi wa mapema na matibabu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *