Uganda yaomboleza afisa wa kwanza kabisa wa kike wa polisi

Pauline Maniraguha Bangirana ni mmoja wa wanawake wa kwanza wawili waliojiunga na kikosi cha polisi nchini Uganda mwaka 1960.

Marion Bosire
2 Min Read

Taifa la Uganda linaomboleza kifo cha afisa wake wa kwanza kabisa wa kike kwa jina Pauline Maniraguha Bangirana ambaye ameaga akiwa na umri wa miaka 85.

Mkuu wa kitengo cha polisi wa upelelezi wa jinai cha bunge Charles Twiine, ndiye alitoa habari za kifo cha Pauline akimtaja kuwa mwanzilishi katika historia ya polisi nchini Tanzania.

Kupitia mtandao wa X, Twiine alisema Mama Pauline alikiuka vizuizi kadhaa mwaka 1960 na kutayarisha njia kwa wanawake kujiunga na kitengo cha polisi.

Twiine anatumai kwamba mama huyo atapatiwa heshima anayostahili na serikali ya Uganda kwa kuandaliwa mazishi ya kitaifa.

Bangirana na mwingine aitwaye Rukidi, ndio walikuwa maafisa wa kwanza kabisa wa polisi wa kike nchini Uganda mwaka 1960 kabla ya wengine wanane kujiunga nao muda mfupi baadaye.

Akiwa hai alikuwa anapenda sana kuzungumzia changamoto ambazo polisi wa kike hupitia kama vile vikwazo vya kuingia kwenye ndoa na kuwa wajawazito.

Wakati huo maafisa wa polisi nchini humo walilazimika kuomba ruhusa ya kuolewa na ujauzito ulikuwa sababu ya kufutwa kazi.

Mwaka 2022,alizindua tawasifu yake kwa jina “To Be Shrewd Without Appearing A Shrew” kitabu ambacho kinaangazia mapambano ya maafisa wa kwanza wa kike wa polisi.

Anasimulia alivyoolewa baada ya kupatiwa idhini na baadaye akapambana kusalia kazini baada ya kuwa mjamzito.

Msimamizi wake alipendekeza ajiuzulu kulingana na sheria za wakati huo lakini Bangirana akaamua kumwomba Inspekta Jenerali wa wakati huo Erinayo Wilson Oryema, ambaye alimpa mapumziko ya kwenda kujifungua, hatua muhimu katika mageuzi ya maslahi ya polisi wa kike.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *