Ukraine yatilia shaka mpango wa Pasaka wa kusitisha mapigano wa Putin

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy hata hivyo amesisitiza kwamba mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yanaendelea.

Marion Bosire
2 Min Read
Vladmir Putin, Rais wa Urusi

Rais Vladimir Putin jana alitangaza hatua ya kushtukizia ya kusitisha vita kwa ajili ya sikukuu ya pasaka huku Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akisisitiza kwamba mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yanaendelea.

Awali Zelenskyy alikuwa ametaja tangazo la Putin kuwa jaribio jingine la kuchezea maisha ya binadamu akisema, “tahadhari za machambulizi ya angani zinasambaa kote nchini Ukraine”.

Baadaye kiongozi huyo wa Ukraine alisema kupitia mtandao wa X kwamba nchi yake ingefuata makubaliano ya kusitisha mapigano iwapo Urusi iko tayari kuhusika kikweli katika mpangilio wa utulivu kamili bila masharti.

Katika taarifa kupitia runinga Putin aliyekuwa akisema na mkuu wa majeshi ya Urusi Valery Gerasimov alisema, “Leo kuanzia saa 12 jioni hadi usiku wa manane Jumapili, upande wa Urusi umetangaza mpango wa kusitisha mapigano kwa ajili ya pasaka”.

Putin alisema atadhania tu kwamba upande wa Ukraine ungefuata mfano wao kwani matendo yao wakati wa utekelezaji wa mpango huo yangeonyesha utayari wao kwa suluhisho la amani.

Lakini kiongozi huyo wa Urusi alimwambia Gerasimov pia atayarishe wanajeshi kujibu jaribio lolote la kuvuruga mpango huo wa kusitisha mapigano wakati wa pasaka.

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilichapisha kwenye Telegram ujumbe uliosema kwamba mpango wa kusitisha mapigano ulichochewa na ubinadamu na utafuatwa na Urusi iwapo Ukraine pia itaufuata.

Andrii Sybiha ambaye ni waziri wa masuala ya kigeni wa Ukraine alijibu akisema kwamba maneno ya Putin hayawezi kuaminika na kwamba wao wataangalia matendo tu.

Website |  + posts
Share This Article