Mfanyabiashara bilionea, mfadhili na kiongozi wa kidini Aga Khan ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 88.
Habari za kifo chake zimetolewa na kituo chake cha kutoa misaada cha Aga Khan Development Network.
Sultan Karim Aga Khan alikuwa kiongozi wa kidini wa 49 wa kundi la Kiislamu la Ismaili, ambalo uzao wa kundi hilo umetoka moja kwa moja kwa mtume Muhammad.
“Alifariki kwa amani jijini Lisbon, Ureno, akiwa amezungukwa na familia yake,” kilisema kituo chake cha kutoa misaada.
Aga Khan ambaye ni mzaliwa wa Uswizi, pia alikuwa na uraia wa Uingereza na aliishi nchini Ufaransa.
Kituo cha Aga Khan kinaendesha mamia ya biashara ikiwa ni pamoja na hospitali, shule na miradi ya kitamaduni, nyingi zikiwa katika mataifa yanayostawi.
Baadhi ya taasisi hizo ni pamoja na kampuni ya Nation Media Group, Chuo Kikuu cha Aga Khan, hospitali za Aga Khan, benki ya Diamond Trust (DTB), kampuni ya bima ya Jubilee na shule za msingi na upili za Aga Khan.