Msanii wa muziki nchini Tanzania Rajabu Adbul Kahali maarufu kama Harmonize ametangaza kamba amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa eneo la Tandahimba, mkoani Mtwara.
Katika chapisho lake la leo kwenye Instagram, msanii huyo alisema kwamba amesoma sheria za kamati ya maadili ya chama cha CCM na za bunge na ameona kwamba haruhusiwi kuwania.
“Nimepitia Sheria za Kamati Yaa Maadili Ya Chama & Bunge Simuoni KONDEBOY. Kwa ninavyoona Hata Kusema BOMBOCLAAAATY Sitoruhusiwa” alitania Harmonize.
Msanii huyo hata hivyo amepongeza wote ambao wamejitokeza kutangaza nia ya kuwania nyadhifa mbali mbali hasa vijana huku akipigia debe chama cha CCM.
Harmonize amewataka wakazi wa Tandahimba wachague kiongozi bora ambaye atasaidiana na Rais Samia kwa miaka mitano ijayo ikifafanua kwamba yeye kwa sasa ana njaa ya ufanisi katika muziki.
Yapata wiki moja iliyopita msanii huyo alitangaza nia ya kuwania ubunge wa eneo alikozaliwa la Tandahimba katika mkoa wa Mtwara huku akichapisha video ya Hayati Magufuli akimpendekeza kwa wadhifa huo.
Huenda msanii huyo hakuwa na nia ya kuingilia siasa bali alitaka aangaziwe zaidi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari ili kutangaza wimbo wake mpya aliomshirikisha msanii wa Nigeria, King Rudy.
Wimbo huo uitwao “Best Couple” ulichapishwa kwenye mtandao wa YouTube siku tatu zilizopita na kufikia sasa umetizamwa zaidi ya mara laki tano.