Serikali na wadau wa ubunifu wahimiza ushirikiano

Wazo hilo lilitolewa na mkurugenzi wa Filamu katika Idara ya masuala ya vijana na uchumi wa ubunifu, kwenye kongamano la Behind the Scenes

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali na wadau wa sekta ya ubunifu wametakiwa kuimarisha ushirikiano ili kukabiliana na changamoto zinazokabili wanawake vijana na wabunifu wengine chipukizi katika sekta ya ubunifu nchini Kenya.

Akizungumza katika kongamano la Behind the Scenes, Mkurugenzi wa masuala ya Filamu katika Idara ya masuala ya vijana na uchumi wa ubunifu, alishiriki jopo lililoongoza mjadala ulioangazia hali halisi inayokabili vijana wa kike katika sekta hiyo.

Mjadala huo uliangazia changamoto kama ukosefu wa mikataba rasmi, uelewa mdogo kuhusu hakimiliki za ubunifu, unyonyaji na ulinzi duni kwa wabunifu wanaofanya kazi kwa kujitegemea.

Otiende alieleza juhudi za serikali kukabiliana na changamoto hizo kupitia sera na mifumo muhimu ya kisheria, kama mswada wa Uchumi wa Ubunifu, Mswada wa hakimiliki wa mwaka 2026 na Muswada wa Vijana.

Alisema hatua hizo zinalenga kuimarisha uchumi wa ubunifu nchini Kenya, kulinda wabunifu na kujenga mazingira wezeshi kwa vijana kupata kipato cha heshima kupitia vipaji vyao.

Otiende pia alisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kijamii yanayohusisha serikali, wabunifu, wadau wa sekta na washirika wengine.

Alisema ushirikiano unaweza kusaidia kuziba mapengo yaliyopo na kupata suluhisho za vitendo, akisisitiza kuwa serikali na wabunifu hawapingani.

Kwa pamoja, alisema, wadau wanaweza kujenga uchumi wa ubunifu wenye nguvu, usawa na ujumuishi zaidi, ambapo vipaji vinalindwa na fursa zinapatikana kwa wote.

Share This Article