Wachimbaji madini nchini Tanzania kupitia Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania, FEMATA wameonyesha nia ya kuanzisha benki.
Tayari mikakati imeanzishwa ili kuafikia mpango huo kama vile uteuzi wa kamati ya kufanikisha ndoto hiyo, hatua iliyochukuliwa na Rais wa FEMATA John Binna.
Binna vile vile amemteua makamu wake Victor Tesha, kuwa mshauri mtaalamu katika mchakato wa kuasisi benki hiyo.
Wachimbaji hao wana bahati kwani tayari, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,BoT, Emmanuel Tutuba, ameridhia kuanzishwa kwa benki maalum ya wachimbaji wa madini nchini Tanzania.
Wazo hili limekuwepo FEMATA kwa muda mrefu ambapo mwaka 2022 ilionekana kwamba liko karibu kabisa kutimia, wachimbaji madini wakichochewa na haja ya kuwa na taasisi ya kifedha inayoweza kutegemewa nao.
Akizungumza baada ya kukutana na wachimbaji wa madini kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Tesha alielezea kwamba amejitolea kuendelea kuwa sauti ya wachimbaji na kusukuma mbele mifumo itakayowawezesha kupata mitaji, teknolojia na huduma za kifedha zinazoendana na mahitaji halisi ya sekta ya madini.
Tesha alisema mshikamano kati ya uongozi wa FEMATA na wanachama wake ni muhimu katika kuimarisha taasisi hiyo ili iwe sauti yenye nguvu na kuleta matokeo chanya kwa wachimbaji wa madini.